>

SIMBA KAZI INAENDELEA, MAELEKEZO KUFUATWA

WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye anga la kimataifa Simba kazi inaendelea kwa kuendelea na mazoezi kambini kuelekea msimu wa 2024/25.

Msimu wa 2023/24 Simba iligotea nafasi ya tatu ikiwa na pointi 69 baada ya kucheza mechi 30 ina kibarua cha kupeperusha bendera ya Tanzania kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.

Beki wa kati Che Malone amesema kuwa wanaamini kupitia maelekezo ya benchi la ufundi watafanya vizuri kwenye mechi zao za ushindani kitaifa na kimataifa.

Che Malone amesema:“Tupo tayari kwa ajili ya msimu ujao na tunaamini kwamba ushindani utakuwa mkubwa kikubwa ambacho tunakifanya kwa sasa ni kufuata maelekezo kutoka kwenye benchi la ufundi kwa kila mchezaji kuwa tayari.

“Ushindani wa msimu ujao utakuwa mgumu hilo tunalitambua jambo ambalo linatufanya tuendelee kuwa makini. Tunaamini itakuwa hivyo mashabiki wazidi kuwa pamoja nasi.”

Simba Day inatarajiwa kuwa Agosti 3 2024 ambapo wachezaji wa msimu wa 2023/24 watatambulishwa ndani ya kikosi na wale wapya pia watatambulishwa siku hiyo.

Wachezaji waliopo Misri kambini ni pamoja na Mohamed Hussen, Shomari Kapombe, Duchu, Ally Salim, Ayoub Lakred, Mzamiru Yassin, Fabrince Ngoma.