KAZI INAENDELEA HUKO MISRI, BENCHI LA UFUNDI LAWASILI

KUELEKEA msimu wa 2024/25 wa Ligi Kuu Bara unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa tayari benchi la ufundi limewasili kambini kuendelea na maandalizi.

Ipo wazi kuwa kwa sasa timu zote Bongo zipo kwenye maandalizi kuelekea msimu mpya unaosubiriwa kwa shauku kubwa, Yanga ambao ni mabingwa watetezi na Azam FC hizi zipo Bongo huku Coastal Union ikiwa inashiriki Kombe la Kagame hizi nne zitapeperusha bendera ya Tanzania kwenye anga la kimataifa.

 Fadlu Davids ambaye ni kocha mkuu, kocha msaidizi, Darian Wilken, mchambuzi wa video, Mueez Kajee na kocha wa Viungo, Riedoh Berdien hawa tayari wapo Misri baada ya kuwasili kambini Julai 10.

Mwamba Selemani Matola ambaye ni kocha msaidizi aliwapokea wageni hao kwa ajili ya kuendelea na kazi ya kukisuka kikosi hicho kitakachopeperusha bendera ya Tanzania kwenye Kombe la Shirikisho katika anga la kimataifa.

Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba amebainisha kwamba wapo tayari kuelekea msimu mpya na wanaamini watafanya vizuri kwenye mashindano ambayo watashiriki.

“Maandalizi mazuri kuelekea msimu mpya tunaamini kwamba tutafanya kazi kubwa kupata matokeo kwenye mashindano ambayo tutashiriki mashabiki wazidi kuwa pamoja nasi.”