>

KIUNGO WA KAZI NGUMU KUSEPA SIMBA, KOCHA MPYA KAZI IPO

INAELEZWA kuwa kiungo wa kazi ngumu ndani ya Simba Sadio Kanoute huenda akasepa ndani ya kikosi hicho kuelekea msimu wa 2024/25.

Kanoute ni mtaalamu kwenye kutembeza mikato ya kimyakimya licha ya sura yake ya upole anatimiza majukumu yake kwa umakini mwanzo mwisho.

Inaelezwa kuwa Kanoute raia wa Mali anahitaji kupata changamoto mpya na anahitaji maboresho ya mkataba wake ndani ya Simba ikiwa wanahitaji huduma yake.

Ni milioni 550 nyota huyo anatajwa kuzihitaji ili asaini dili jipya pamoja na mshahara mkubwa jambo linaloongeza nafasi kwake kusepa.

Wakati hayo yakitokea Julai 5 2024 Simba  ilimtangaza Fadlu Davids, raia wa Afrika Kusini, kuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo akipewa mkataba wa miaka miwili.

Nyota huyo wa zamani wa soka nchini Afrika Kusini mwenye miaka 43, alikuwa Kocha Msaidizi wa Raja Casablanca ya nchini Morocco.

Simba inatarajia kuweka kambi Misri ikiwa ni maandalizi ya msimu mpya wa 2024/25 ambao unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kwa kila timu kupambania kombe.