MANCHESTER UNITED IPO TAYARI KUSIKILIZA OFA KWA AJILI YA MARCUS RASHFORD

Manchester United ipo tayari kusikiliza ofa kwa ajili ya Marcus Rashford baada ya kuvunjika kwa uhusiano wa mshambuliaji huyo na Meneja Erik ten Hag huku PSG ikitajwa kuhitaji saini ya nyota huyo raia wa England.

Kwa mujibu wa ripoti ilikuwa ni mmoja kati ya Rashford au Ten Hag ambaye alihusishwa kutimka klabuni hapo kutokana na mpasuko kati ya pande hizo mbili lakini kwa sasa ni wazi Rashford anasalia kuwa ‘kondoo wa kafara’ baada ya uamuzi wa Man United kumbakisha Ten Hag.

Inaripotiwa kuwa Mashetani hao Wekundu wanahitaji kitita cha pauni milioni 80 kwa ajili ya mhitimu huyo ya shule ya vipaji ya klabu hiyo lakini huenda ikalazimika kukubali pauni milioni 60 baada ya fowadi huyo kuwa msimu usioridhisha msimu uliopita.

Rashford haziivi na Ten Hag tangu mwishoni mwa msimu uliopita baada ya kuonekana kufanya tafrija kwenye ‘night club’ mjini Belfast wakati alitakiwa kuwa kwenye mazoezi ya klabu hiyo kuelekea mchezo wa kombe la FA dhidi ya Newport ambao hakucheza.