MABINGWA wa CRDB Federation Cup Yanga wameanza hesabu kuelekea mchezo wao wa fainali dhidi ya Azam FC inayonolewa na Kocha Mkuu Yusuph Dabo.
Ipo wazi kwamba Mei 30 kikosi cha Yanga kinachonolewa na Kocha Mkuu, Miguel Gamondi kilitia timu ndani ya Zanzibar kwa ajili ya maandalizi ya mchezo huo ujao.
Ukiweka kando kuwa na taji la ligi Yanga wanapiga hesabu za kutwaa taji hilo ambalo wanalitetea kwa kuwa walitwaa mbele ya Azam FC fainali ya Tanga, Uwanja wa Mkwani.
Kwenye fainali inatarajiwa pia tuzo za Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF) kwa wachezaji walioshiriki Ligi Kuu Bara msimu wa 2023/24 kutolewa pia baada ya fainali.
Miongoni mwa tuzo ambazo zinapigiwa hesabu kubwa ni ile ya MVP ambapo majina ya wachezaji wawili Feisal Salum wa Azam na Aziz KI wa Yanga yanatajwa kuwa miongoni mwa wale ambao wataibuka na tuzo hiyo kubwa.
Bakari Mwamnyeto, nahodha wa Yanga amebainisha kuwa wapo tayari kwa mchezo huo kwa kuwa tayari maandalizi yameanza.
“Tupo tayari kwa fainali na si asilimia 100 ni asilimia elfu moja, maandalizi yapo sawa na tunaamini kwamba tunakwenda kulitetea taji.”.
Fainali inatarajiwa kuchezwa Uwanja wa New Amaan Complex, Juni 2 2024.