WAJUE WAWAKILISHI WA KIMATAIFA

PAZIA la Ligi Kuu Bara msimu wa 2023/24 limefungwa kwa kila timu kujua ilivuna nini baada ya kupanda kwenye mechi 30 ambazo ni dakika 2,700 za jasho kuvuja kupata matokeo chanya ndani ya uwanja.

Hakuna ambaye alikuwa hana mpango wa kutwaa taji la ligi ila ipo wazi ni lazima mshindi awe mmoja katika timu 16 shiriki ni Yanga kawazidi wote akiwa na pointi 80 akitwaa taji la ligi kwa msimu uliogota mwisho.

Ikumbukwe kwamba alitangazwa kuwa bingwa akiwa amecheza mechi 27 mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar alipovuna pointi tatu akafikisha jumla ya pointi 71 ambazo hazijafikiwa na timu yoyote mpaka msimu unagota mwisho Mei 28 2024.

Kwenye anga la kimataifa kuna timu nne ambazo zinakwenda kupeperusha bendera ya Tanzania katika kusaka ushindi huko katika Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika.

Ipo namna hii timu inayomaliza nafasi ya kwanza nay a pili hizo moja kwa moja ni kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na nafasi ya tatu mpaka ya nne hizo ni Kombe la Shirikisho Afrika.

Ni Yanga inayonolewa na Kocha Mkuu Miguel Gamondi ikiwa namba moja na pointi 80 baada ya mechi 30 itashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika na ikumbukwe kwamba msimu wa 2023/24 iligotea hatua ya robo fainali.

Azam FC matajiri wa Dar hawa wamegotea nafasi ya pili kwenye msimamo wakiwa na pointi 69 kibindoni, nao wanapeperusha bendera ya Tanzania kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

Msimu wa 2023/24 ilishiriki Kombe la Shirikisho hivyo imepiga hatua moja nyingine mpaka kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika msimu mpya wa 2024/25 kwa matajiri hao wa Dar, chini ya Kocha Mkuu, Yusuph Dabo.

Simba inayonolewa na Kocha Mkuu, Juma Mgunda imeporomoka nafasi moja iliyogotea msimu wa 2022/23 sasa ni nafasi ya tatu hivyo ni Kombe la Shirikisho itakuwa kupambanania nembo ya Tanzania.

Ni pointi 69 ilimaliza nazo kwenye msimu sawa na Azam FC wakijenga ukuta kwenye idara ya mabao ya kufunga na kufungwa. Azam FC ilifunga jumla ya mabao 63 na Simba mabao 59 kwa upande wa kufungwa ni mabao 21 Azam ilifungwa na Simba ilifungwa mabao 25.

Coastal Union inayotumia Uwanja wa Mkwakwani, Tanga kwa mechi za nyumbani haikuanza kwenye mwendo mzuri msimu wa 2023/24 lakini imemaliza ikiwa ndani ya nne bora.

Nafasi ya nne na pointi 43 zinaipa tiketi timu hiyo kuwa kwenye anga la kimataifa ambapo itaonyesha nguvu yake kwenye Kombe la Shirikisho Afrika katika kupeperusha bendera ya Tanzania kimataifa.