MABINGWA wa Ligi Kuu Bara, Yanga msimu wa 2023/24 wamebainisha kuwa moja ya malengo yaliyopo ni kupata ushindi kwenye mchezo wao dhidi ya Tabora United.
Leo Mei 25 Yanga inayonolewa na Kocha Mkuu Miguel Gamondi inakibarua cha kusaka pointi tatu dhidi ya Tabora United.
Mchezo huo ni maalumu kwa Yanga kukabidhiwa taji la ligi ambalo walitwaa walipofikisha pointi 71 wakiwa wamecheza mechi 27 na kubakiwa na michezo mitatu.
Kwa sasa ni namba moja ikiwa na pointi 74 baada ya kucheza mechi 28 leo ni mchezo wa 29 unatarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mkapa saa 10:00 jioni.
Gamondi amesema: “Moja ya malengo niliyoweka baada kushinda ubingwa, ni kushinda mechi tatu zinazofuata kwa kuwa tunatambua kwamba ni muhimu kupata matokeo mazuri.
“Mashabiki wajitokeze kwa wingi kupata burudani kwa kuwa wamekuwa pamoja nasi kwenye mechi zote ambazo tulikuwa tunacheza nyumbani na ugenini pia.”
Beki Ibrahim Abdallah ‘Bacca’ amesema fikra zao ni ushindi kwanza na sio sherehe za ubingwa. Baada ya mechi ndio watasheherekea.