YANGA WAIPA TANO SPORTPESA KWA KUWATOA KWENYE MAGUMU

Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said ameweka wazi kuwa ndani ya miaka saba wakiwa na udhamini wa SportPesa wamefanya mengi ambayo yanaingia katika sehemu ya mafanikio.

Rais huyo amebainisha kuwa kampuni ya SportPesa imewatoa Yanga kwenye wakati mgumu ambapo hawakuwa na mdhamini yoyote hivyo wakafanya mengi makubwa ndani ya miaka mitano na mkataba ulipoisha kampuni ya SportPesa na Yanga walikubaliana kuendelea kwa mara nyingine tena.

Ipo wazi kuwa Yanga ni mabingwa wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2923/24 wakiwa na pointi 71 baada ya kucheza mechi 27.

Injinia amesema: “Ninayo furaha kutoa historia ya safari ya miaka saba kati ya Yanga na taasisi ya SportPesa, safari imekuwa na mafanikio makubwa. Makubaliano kati ya Yanga na SportPesa yalifanyika kwa mkataba wa miaka mitano.

“Tukumbuke wakati huo Yanga haikuwa na mdhamini kabisa ilikuwa katika wakati mgumu wa kifedha hivyo mkataba wa SportPesa na Yanga ulituinua na kutupa nafasi ya kufanya maboresho na usajili kwa ajili ya wachezaji.
“SportPesa alikuwa mkombozi wetu hatimaye Yanga ikaanza kurejea katika ubora wake. SportPesa walitupa nguvu akiwa ni mdhamini mkuu.

Baada ya mkataba wa miaka mitano kuisha SportPesa na Yanga tuliingia mkataba mwingine wa miaka mitatu hapo makubaliano mengine yalikubalika na hapo Yanga ilianza kuwa imara na tukiweza kuchukua ubingwa wa ligi back to back na FA back to back ndani ya miaka miwili na sasa tukiwa na SportPesa tumetwaa taji la ligi ikiwa ni mara ya 30.”