BENCHI la ufundi la Simba limebainisha kuwa maandalizi yanaanza kuelekea mchezo wao ujao dhidi ya Dodoma Jiji unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
Ipo wazi kwamba mchezo huo awali ulipangwa kuchezwa Mei 16 2024 lakini umepangiwa tarehe mpya ambayo itakuwa ni Mei 17 2024.
Mchezo uliopita Simba chini ya Juma Mgunda akishirikiana na Seleman Matola iligawana pointi mojamoja na Kagera Sugar kwa kushuhudia ubao wa Uwanja wa Kaitaba ukisoma Kagera Sugar 1-1 Simba.
Bao la Simba lilifungwa na Ladack Chasambi na lile la Kagera Sugar lilifungwa na Obrey Chirwa.
Mgunda amesema; “Makosa ambayo yamepita tunyafanyia kazi kwa ajili ya kuona kwamba mechi zijazo tunapata matokeo mazuri, kikubwa ni kuona kila mchezaji anatimiza majukumu yake.
“Wachezaji wapo tayari na ni muda wa kupambana kufanya vizuri kwenye mechi zetu zilizobaki kwa kuwa hakuna mchezaji ambaye hapendi kufunga.”.
Simba ipo nafasi ya tatu kwenye msimamo ina pointi 57 inakutana na Dodoma Jiji iliyo nafasi ya 11 na pointi 30.