YANGA WANA BALAA HAO, SIRI HII HAPA

NDANI ya Ligi Kuu Bara Yanga ni baba lao kutokana na kasi yao ya kusaka matokeo kwenye mechi za Ligi Kuu Bara ikiwa inaongoza ligi baada ya kucheza jumla ya mechi ambazo wanacheza.

Mchezo wao uliopita kwenye ligi ilikuwa dhidi ya Kagera Sugar ambao ni mzunguko wa pili ulichezwa Uwanja wa Azam Complex, baada ya dakika 90 ubao ulisoma Yanga 1-0 Kagera Sugar.

Bao pekee la ushindi kwenye mchezo huo lilifungwa na kiungo mshambuliaji Mudathir Yahya ambaye alianzia benchi alipoingia alifanya kazi yake kwa ushirikiano mkubwa na wachezaji wengine.

Ilikuwa dakika ya 83 Mudathir alipachika bao hilo akitumia pasi ya kiungo mshambuliaji Aziz KI ambaye anafikisha jumla ya pasi 8 ndani ya ligi na katupia jumla ya mabao 15.

Ipo wazi kwamba Aziz KI ni chaguo la kwanza la Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi ambaye aliweka wazi kuwa wachezaji wote wa Yanga wanacheza kwa ushirikiano na kila mmoja anatimiza majukumu yake kwa umakini.

“Kikubwa ambacho kinafanyika kwenye mechi ambazo tunacheza ni umakini na kila mchezaji anatimiza majukumu yake kwa ushirikiano na wachezaji wengine hilo ni jambo kubwa.

“Muhimu ni kuona kwamba tunapata matokeo kwani ili kufikia malengo ya kutwaa ubingwa wa ligi ni muhimu kushinda na kupata pointi tatu ambazo tunatambua kwamba na wapinzani wetu wanazihitaji pia.”

Gamondi ana tuzo ya kocha bora wa ligi kwa Aprili sawa na mchezaji wa timu hiyo Aziz KI ambaye mguu wake wenye nguvu ni ule wa kushoto ukiwa umefunga mabao 13 na ule wa kulia katupia mabao mawili.

Kwa upande wa Aziz KI amebainisha kwamba malengo makubwa ni kuona wanapata ushindi kwenye mechi ambazo wanacheza hilo ni jambo la kwanza kisha mengine yatafuata.

“Sifikirii kuhusu tuzo yangu binafsi bali kwanza timu halafu mengine yatafuata kikubwa kinachotupa ushindi ni ushirikiano mashabiki wazidi kuwa pamoja nasi.”