>

WACHEZAJI YANGA HAWADAIWA, WAPEWA KAZI NYINGINE KIMATAIFA

MIGUEL Gamondi, Kocha Mkuu wa Yanga amebainisha kwamba kwa namna ambavyo wachezaji wake wamejitoa mbele ya wapinzani wao Mamelodi Sundowns hana cha kuwadai zaidi ya kufanyia kazi makosa yao.

Machi 30 2024 ubao wa Uwanja wa Mkapa kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya dakika 90 ulisoma Yanga 0-0 Mamelodi Sundowns kwenye hatua ya robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika.

Gamondi amesema:  “Siwadai wachezaji wangu hakika wamecheza vyema na kufuata maelekezo, tumekutana na timu kubwa na bora ambayo inauzoefu na hii michuano hii mikubwa Afrika.
“Ukiwa mwalimu na wachezaji wakawa wanacheza kwa kufuata maelekezo yako basi unafurahia na ndio furaha nlioipata hata kama hatujapata matokeo.

“Kwa sasa tunaenda ugenini tukiwa na matumaini ya wachezaji wengine ambao walikosekana kurejea na ukweli ni kwamba natamani tucheze fainali msimu huu hivyo tunaamini kwamba tutapambana kufanya vizuri,”.