UONGOZI wa Klabu ya Tabora United umefikia makubaliano ya pande zote mbili ya kusitisha mkataba na aliyekuwa Kocha Mkuu Goran Copnovic raia wa Serbia.Rasmi leo Machi 21 2024 taarifa imetolewa baada ya awali tetesi kueleza kuwa kocha huyo amesitishiwa mkataba wake kutokana na mwendo mbovo wa timu hiyo.
Tabora United imefikia uamuzi huo kutokana na kutorodhishwa na mwenendo wa matokeo ambayo timu hiyo imekuwa ikiyapata katika michezo yake ya Ligi Kuu ya NBC, Tanzania Bara.
Goran Copnovic alijiunga na Tabora United Agosti mwaka 2023 kama kocha mkuu kwa mkataba wa mwaka mmoja ambao ulikuwa umalizike mwishoni mwa msimu huu kabla ya kufikia uamuzi wa kuvunjwa mapema leo hii.
Taarifa iliyotolewa na Christina Mwagala, Ofisa Habari wa Tabora United imebainisha kwamba wanatambua mchango wa kocha huyo na kumuombea kila la kheri.”Tabora United inamshukuru kocha Goran kwa utumishi wake tangu alipojiunga na timu na hivyo inamtakia kila la kheri huko aendako,”.Mchezo wa mwisho kwa kocha huyo ilikuwa ni dhidi ya KMC ubao wa Uwanja wa Azam Complex, Machi 10 uliposoma KMC 4-2 Tabora United.