MUDA ASEPA NA TUZO YAKE FEBRUARI

KIUNGO wa Yanga ambaye mtindo wake wa ushangiliaji kila anapofunga ni kuonekana kama anaongea na simu amechaguliwa kuwa mchezaji bora ndani ya kikosi cha Yanga kwa Februari.

Ni Mudathir Yahya ambaye katupia jumla ya mabao 8 ndani ya Ligi Kuu Bara msimu wa 2023/24 amekuwa chaguo la kwanza la Kocha Mkuu, Miguel Gamondi kwenye mechi za hivi karibuni.

Nyota huyo amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa Yanga kwa mwezi Februari akiwashinda Pacome Zouzoua na Nickson Kibabage ambao aliingia nao fainali kwenye tuzo hiyo inayodhaminiwa na NIC.

Mudathir amewaka ambapo katika mechi mbili mfululizo zilizopita dhidi ya Namungo FC na dhidi ya Ihefu SC  Uwanja wa Azam Complex alifunga akikamilisha mabao 8.

Machi 14 kikosi cha Yanga kinatarajiwa kuwa na mchezo wa ligi Uwanja wa Azam Complex, dhidi ya Geita Gold.