YANGA YAZITAKA POINTI TATU ZA IHEFU

KOCHA Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi amesema kuwa wataingia kwa tahadhari kuwakabili wapinzani wao Ihefu kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Azam Complex.

Machi 11 Yanga ambao wametoka kushuhudia ubao wa Uwanja wa Majaliwa ukisoma Namungo 1-3 Yanga watakuwa na kazi ya kusaka pointi tatu dhidi ya Ihefu.

Katika mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Highland Estate baada ya dakika 90 ubao ulisoma Ihefu 2-1 Yanga ikiwa ni mchezo wa kwanza kwa vinara hao kupoteza ndani ya msimu wa 2023/24.

Gamondi ameweka wazi kuwa kikubwa ambacho wanahitaji kwenye mchezo wao dhidi ya Ihefu ni pointi tatu muhimu.

“Tunatambua hautakuwa mchezo mwepesi lakini tupo tayari kutokana na maandalizi ambayo tumefanya na kikubwa ni kuona kwamba tunapata pointi tatu kwenye mchezo wetu.

“Mashabiki wajitokeze kwa wingi kupata burudani kwenye mchezo wetu ukizingatia kwamba tutakuwa nyumbani ni muda wa kuendelea kufanya vizuri,”.

Yanga ni vinara wa ligi wakiwa na pointi 46 baada ya kucheza mechi 17 wanakutana na Ihefu yenye pointi 23 baada ya kucheza mechi 19.