HII HAPA SABABU YA YANGA KUJA NA PACOME DAY

UONGOZI wa Yanga umeweka wazi kuwa sababu kubwa ya kuja na Pacome Day Kitaalamu Zaidi inatokana na utaalamu wa kiungo huyo kwenye eneo la kiungo mshambuliaji ndani ya uwanja kuwapoteza wachezaji wengi wa timu pinzani.

Ipo wazi kwamba ndani ya Ligi Kuu Bara, Pacome kafunga mabao sita na pasi tatu za mabao katika Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi katupia jumla ya mabao matatu akiwa ni namba moja kwa watupiaji upande wa Yanga na namba mbili kwa Afrika.

Ali Kamwe, Ofisa Habari wa Yanga amesema kuwa kuelekea mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya CR Belouizdad itakuwa ni Pacome Day Kitaalamu Zaidi na wataonyesha utaalamu wenye kila idara.

“Pacome ni mchezaji bora ambaye kwenye eneo la kiungo anacheza kitaalamu zaidi kuliko wapinzni wetu na pia anaongoza kwenye idadi ya kufunga mabao kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika akiwa nayo matatu, hautaki unataka itabaki kuwa hivyo.

“Wachezaji wote ndani ya Yanga ni wataalamu kuna Dickson Job, Maxi Nzengeli, Aziz KI, Djigui Diarra kila mchezaji ana utalaamu wake mpaka mashabiki, viongozi sasa kwa nini isiwe Kitaalamu Zaidi.

“Mashabiki wajitokeze kwa wingi na ule atakayetokelezea zaidi kuanzia kichwani kwa kuwa kama Pacome na bleach hakika atapewa zawadi na unajua kwamba zawadi zetu huwa ni zawadi hasa kutoka kwa GSM,”.

Mchezo huo wa kundi D unatarajiwa kuchezwa saa 1:00 usiku Uwanja wa Mkapa ambapo timu zote baada ya kucheza mechi tatu zimekusanya jumla ya pointi tano, vinara ni Al Ahly wenye pointi sita.

Yanga inatarajiwa kucheza leo mchezo wa raundi ya tatu wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Polisi Tanzania saa 1:00 usiku, Uwanja wa Azam Complex.