GAMONDI AMKOMALIA JOB

MIGUEL Gamondi, Kocha Mkuu wa Yanga ameweka wazi kuwa ni lazima safu yake ya ulinzi kuhakikisha inakuwa kwenye mwendo bora kila wakati katika mechi za ushindani ili kuongeza nguvu ya kupata ushindi.

Katika safu ya ulinzi ya Yanga chaguo namba moja kwa Gamondi ni Dickson Job beki mwenye rekodi ya kuwa mfungaji wa bao la kwanza ndani ya kikosi hicho ilikuwa dhidi ya KMC mchezo uliochezwa Uwanja wa Azam Complex.

 Yanga ni namba moja kwa timu zilizoruhusu mabao machache ya kufungwa ambayo ni sita kwenye ligi baada ya kucheza mechi 13 ikiwa nafasi ya kwanza kwenye msimamo na pointi 34.

 Gamondi amesema kuwa ni muhimu kwa wachezaji wote kucheza kwa ushirikiano kwenye kutimiza majukumu yao ikiwa ni kuzuia kufungwa na kufunga mabao kwenye mechi zao.

“Tuna kazi kubwa ya kufanya kwenye kila idara kuanzia ile ya ulinzi ambayo ni muhimu kuhakikisha kwamba hatufungwi kwenye kila mchezo hiyo itatupa nguvu kutafuta mabao mengi kushinda.

“Ni rahisi kuwa kwenye mwendo mzuri pale ambapo unakuwa na timu ambayo haifungwi lakini ikitokea mkifungwa hapo presha inakuwa kubwa kwenye kutafuta mabao mengine zaidi kupata ushindi. Nina amini wachezaji wanafanya kazi nzuri wanapaswa kuendelea,” alisema Gamondi.

Mbali na Job ukuta wa Yanga unaongozwa na nahodha Bakari Mwamnyeto na kitasa mwingine ni Ibrahim Bacca beki wa kupanda na kushuka.