TAIFA STARS KAZINI LEO AFCON

HATIMAYE baada ya Januari 13 2024 kazi kuanza kufanyika Ivory Coast kwenye mashindano makubwa barani Afrika, Kombe la Mataifa Afrika maarufu kama AFCON leo ni zamu ya Tanzania kutupa kete yake ya kusaka ushindi.

Kuelekea kwenye mchezo huo kocha msaidizi wa timu ya taifa ya Tanzania, Hemed Morocco amesema kuwa wachezaji wapo tayari kupambana na kupata ushindi kwenye mchezo dhidi ya timu ya taifa ya Morocco.

Huu ni mchezo wa kwanza kwa Taifa Stars ambayo ipo Ivory Coast kwa ajili ya kupeperusha bendera ya Tanzania kwenye mashindano makubwa Afrika ya AFCON.

Ikumbukwe kwamba mabingwa watetezi wa taji la AFCON ni Senegal yenye Sadio Mane mchezo wao wa kwanza walipata ushindi wa mabao 3-0 Gambia.

Morocco amesema kuwa wanatambua ugumu kuwakabili wapinzani wao lakini walishawahi kucheza nao hivyo  wanatambua namna bora ya kuwakabili kupata matokeo chanya.

Tumekuwa na muda mzuri wa kufanyia kazi makosa yalitokea kwenye mechi za kirafiki pamoja na mechi zilizopita hivyo kwenye uwanja wa mazoezi tulikuwa imara kuwa bora kwa ajili ya mechi zinazofuata.

Mchezo wetu dhidi ya Morocco tunatambua kwamba utakuwa mgumu ila tupo tayari na wachezaji wanatambua kwamba tunahitaji ushindi kwenye mchezo huo muhimu,” alisema Morocco.

Ipo wazi kuwa Januari 16 wachezaji wa timu ya taifa ya Tanzania ikiwa ni pamoja na Mbwana Samatta, Feisal Salum, Mzamiru Yassin walipata nafasi ya kuutembelea uwanja wa Laurent Pokou (Stade Laurent Pokou) utakaotumika kwa mchezo wao dhidi ya Morocco.

Mechi hiyo itaanza saa 2:00 usiku ambapo timu zote zitakuwa kazini kusaka ushindi ndani ya dakika 90.