LUIS KAZI YAKE IPO HIVI MAPINDUZI 2024

KIUNGO wa Simba, Luis Miquissone ni habari nyingine ndani ya Mapinduzi 2024 kutokana na kuwa na zali la kuhusika kwenye miguso iliyoleta mabao katika timu hiyo.

Ni pasi tatu za mabao  katoa na kufunga bao moja. Januari Mosi dhidi ya JKU alifanya kweli kwa kutengeneza pasi mbili za mabao ile ya kwanza alimpa Moses Phiri dakika ya 8 na ile ya pili alitoa krosi chonganishi dakika ya 64 ikakutana na beki Mohamed Hassan ambaye alijifunga.

Katika mchezo huo mwisho ubao wa Amaan ulisoma JKU 1-3 Simba huku lile bao la tatu likifungwa na ingizo jipya Saleh Karabaka kutoka JKU alipowaadhibu mabosi wake wa zamani.

Hakugotea hapo kwenye kutoa pasi pekee alifunga bao moja ilikuwa kwenye mchezo dhidi ya Singida Fountain Gate akitumia pasi ya Shomari Kapombe, baada ya kufunga bao hakushangilia, alirejea uwanjani kuendelea na majukumu yake.

Pasi ya tatu ilikuwa kwenye mchezo wa hatua ya robo fainali Januari 8 alitoa kwa Jean Baleke dakika ya 45+3 ambapo akiwa nje ya 18 alikutana na krosi ya Fabrince Ngoma aliyechaguliwa kuwa mchezaji bora kwenye mchezo huo.

Simba ikiwa imecheza mechi tano, tatu za hatua ya makundi na moja ya robo fainali na moja nusu fainali ni mabao saba imefunga huku safu ya ulinzi ikiokota mabao mawili na Luis kahusika kwenye mabao manne.

Januari 13 ni fainali Mlandege ambao ni mabingwa watetezi dhidi ya Simba.