MSENEGAL Bababacar Sarr kiungo mpya wa Simba ameanza balaa lake ndani ya Mapinduzi 2024 kwa kuonyesha kile kilichopo kwenye miguu yake.
Nyota huyo anayetajwa kuwa na uwezo wa kucheza nafasi zaidi ya mbili uwanjani ikiwa ni kiungo mkabaji na kiungo wa kata alitambulishwa rasmi Januari 6 kujiunga na Simba inayonolewa na Kocha Mkuu, Abdelhack Benchikha.
Mchezo wake wa kwanza akiwa na uzi wa Simba ilikuwa ni Januari 8 kwenye hatua ya robo fainali Mapinduzi 2024 dhidi ya Jamhuri baada ya dakika 90 ubao wa Uwanja wa Amaan ulisoma Simba 1-0 Jamhuri. Jean Baleke alifunga dakika ya 45+3.
Sarri alikomba dakika 20 kwenye mchezo huo ambao Jamhuri waliingia uwanjani kwa mbinu za kujilinda zaidi alichukua nafasi ya Saido Ntibanzokiza.
Katika dakika hizo alizoingia alionekana ni mwenye kujiamini huku akitumia mguu wa kulia kutoa pasi zake nyingi ambazo zilikuwa ni fupi na ndefu huku akipiga pasi zaidi ya 15 zilizowafikia walengwa.
Alipiga pasi fupi dakika ya 71, 81, 72, 73, 76, 80, 85, 87, zile ndefu ilikuwa dakika ya 72, 82, 83, 90 alicheza faulo dakika ya 76 alionesha uwezo wa kukokota dakika 77 alipewa jukumu la kupiga faulo dakika 80.
Leo Simba inatarajiwa kuwa na kibarua cha kusaka ushindi kwenye mchezo wa nusu fainali dhidi ya Singida Fountain Gate na mshindi atakutana na Mlandege ambao ni mabingwa watetezi hatua ya fainali.