UKIWA ni mchezo wake wa kwanza akiwa na kikosi cha Simba, Saleh Karabaka alifungua ukurasa wake wa mabao katika Mapinduzi Cup 2024.
Ingizo hilo jipya dirisha dogo alikuwa anakipiga JKU hivyo alianza kazi mbele ya mabosi wake wa zamani akisaini dili la miaka mitatu.
Baada ya dakika 90 ubao ulisoma JKU 1-3 Simba ambapo ni Neva Kaboma alipita katikati ya ukuta wa Simba dakika ya 41 na kupachika bao la kufutia machozi.
Moses Phiri alifungua pazia la mabao dakika ya 8 na bao la pili ilikuwa la kujifunga kupitia kwa Mohamed Hassa dakika ya 64 na chuma cha tatu ni Karabaka dakika ya 65.
Karabaka alipewa tuzo ya mchezaji aliyeonyesha kiwango bora kwenye mchezo huo ukiwa ni wa kwanza kwa Simba ndani ya Januri 2024 wakiibuka na ushindi.
Ayoub Lakred kipa wa Simba naye ameanza Januari kwa kutunguliwa kwenye mchezo wake wa kwanza kuanza langoni ndani ya 2024.