MWANDISHI WETU
KOCHA Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, amesema ili Yanga imalize tatizo la straika ndani ya kikosi hicho, wanapaswa kumnunua mchezaji wa eneo hilo mwenye thamani ya shilingi bilioni 2.5.
Gamondi ametoa kauli hiyo baada ya kuwepo kwa maswali mengi juu ya uwezo wa washambuliaji wa Yanga katika kufunga mabao ambapo hivi sasa timu hiyo inategemea zaidi mabao kufungwa na viungo.
Katika kikosi cha Yanga, Stephane Aziz Ki ndiye anaongoza kwa mabao ndani ya Ligi Kuu Bara akifunga 10, akifuatiwa na Maxi Nzengeli (7), kisha Pacome Zouzoua (4), hawa wote ni viungo. Kwa upande wa washambuliaji, Kennedy Musonda amefunga matatu, Hafiz Konkoni (1) na Clement Mzize (1).
Akizungumzia hilo la kuongeza straika kipindi hiki cha dirisha dogo, Gamondi alisema: “Tunatafuta straika lakini lazima uelewe kwamba ni ngumu kumpata aliyebora kipindi hiki, nani anaweza kumuachia straika wake bora kipindi hiki.
“Labda mchezaji awe na matatizo ya mkataba na klabu yake au haelewani na kocha, lakini mchezaji bora kwa sasa huwezi kumpata bure.
“Ukinipa dola kuanzia 100,000 (zaidi ya Sh milioni 250) mpaka dola 1,000,000 (zaidi ya Sh bilioni 2.5) nitamleta straika aliye bora.
“Watu wanalalamika, wanipe hela nilete straika mzuri, ni rahisi kusema. Mchezaji unatakiwa kumfuatilia kwa takribani miezi mitatu, pili fedha lazima itumike.
“Watu wanataka straika akija awe anafunga mabao na si kusubiri, lakini huyohuyo akija anatakiwa kwanza kuzoea mazingira, inakuwa ngumu, mfano anatokea Amerika haijui ligi wala lugha, huwezi moja kwa moja ukamuweka uwanjani akakufungia mabao matatu. Niwaambie tu, hata mimi nalitambua hilo, lakini sio rahisi kupata straika mzuri wamtakaye wao.
“Lakini nina furaha na mbinu zangu ambazo zinafanya kazi vizuri, Aziz Ki anafunga na sasa ni mfungaji bora, Musonda anafunga, Yao anatengeneza nafasi na kufunga, tuna mwendo mzuri sana.”