UONGOZI wa Coastal Unioni, umesema unaendelea kulitumia dirisha hili dogo la usajili kuboresha kikosi chao kwa kuzingatia ripoti ya Kocha Mkuu, David Ouma aliyoiwasilisha mapema kabla ya usajili kufunguliwa Desemba 16, mwaka huu.
Ofisa Habari Coastal Union, Abbas El-Sabry, amesema ripoti ya kocha mkuu imeanza kufanyiwa kazi haraka kwa sababu hakuna muda wa kupoteza, huku akibainisha kwamba baadhi ya wachezaji wameshamalizana na klabu na wengine wanaotarajiwa kusajiliwa wapo katika hatua nzuri za kukamilisha usajili wao.
“Ripoti ya mwalimu aliyoipendekaeza ina baadhi ya majina ya wachezaji wanaocheza Ligi Kuu Bara, Ligi ya Zanzibar na nchi jirani kwa maana ya Kenya na Uganda.
“Kwa hiyo tayari skauti wetu wanapita sehemu mbalimbali kuangalia wachezaji wenye viwango ambavyo mwalimu anahitaji, siku chache zijazo tutaanza kuwajulisha kuhusu wachezaji wanaoingia ndani ya klabu yetu.
“Pia tupo katika mazungumzo na wachezaji wawili ambao ni Fiston Abdulrazak na Salim Aiyee, bado hatujawasajili, lakini tukimalizana mara moja tutawajulisha Wanacoastal.
“Tutakuwa makini katika kuziba nafasi za wachezaji walioondoka, tutasajili kwa umakini kulingana na ripoti ya mwalimu,” alisema El-Sabry.
Baadhi ya wachezaji ambao tayari Coastal Union imetangaza kuachana nao kipindi hiki cha dirisha dogo ni Fran Golubic, Balama Mapinduzi na Juma Mahadhi.