BINGWA MAPINDUZI CUP KULAMBA MAMILIONI

KAMATI ya Kombe la Mapinduzi, imetangaza rasmi kwamba, bingwa wa michuano hiyo ataondoka na kitita cha shilingi milioni 100, huku mshindi wa pili kukabidhiwa shilingi milioni 70.

Mashindano hayo ambayo yanatarajiwa kuanza Desemba 28, mwaka huu, yatashirikisha timu 12, huku msimu uliopita bingwa ambaye alikuwa Mlandege, aliondoka na shilingi milioni 50.

Mwenyeketi wa Kamati ya Mashindano ya Kombe la Mapinduzi, Mbarouk Othman, amesema siku ya ufunguzi, itachezwa michezo miwili kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Amesema timu za Bandari ya Kenya na URA ya Uganda, zimejitoa katika mashindano hayo na nafasi zao zimechukuliwa na Jamuso kutoka Sudan Kusini na JKU ya Zanzibar.

Amesema mara baada ya kufanyika mabadiliko hayo, makundi yatakuwa hivi; Kundi A: Azam, Vital’O, Chipukizi na Mlandege.
Kundi B: Simba, JKU, APR na Singida. Kundi C: Yanga, Jamhuri, JAMUSO na KVZ.

Mbali na hayo, amesema katika mashindano hayo, hatua ya awali viingilio kwa mechi za jioni ni Sh 5000 na Sh 3000, huku mechi za usiku ni Sh 10,000, Sh 5,000 na Sh 3,000. Jukwaa la V.I.P ni Sh 100,000 kwa mechi zote.