>

YANGA KUFANYA KAZI KUBWA

UONGOZI wa Yanga umebainisha kuwa utafanya kazi kubwa kufanikisha malengo ya kutwaa ubingwa ambao upo mikononi mwao waliotwaa msimu wa 2022/23.

Chini ya Miguel Gamondi Yanga ilitoka kupata ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Mtibwa Sugar mchezo uliochezwa Uwanja wa Azam Complex.

Kinara wa utupiaji wa mabao ni Aziz KI ndani ya Yanga na ligi kiujumla akiwa katupia mabao 9 kibindoni ambapo kwenye mabao hayo alifunga hat trick moja kwenye mchezo dhidi ya Azam FC.

Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe alisema kuwa kikubwa ni kufanya vizuri kwenye mechi zote wanazocheza ili kupata matokeo chanya.

“Kikubwa kwenye mechi za ligi tunahitaji matokeo mazuri ambayo yatatufanya tufikie malengo yetu ya kutwaa ubingwa inawezekana kutokana na wachezaji waliopo.

“Benchi la ufundi furaha yao ni kuona matokeo yanapatikana hivyo tu basi. Mashabiki wazidi kuwa pamoja nasi kwenye mechi zote ambazo tunacheza,” alisema Kamwe.

Baada ya kucheza mechi 10 Yanga kibindoni ina jumla ya pointi 27 vinara wakiwa ni Azam FC wenye pointi 28 baada ya kucheza mechi 12.

Mchezo ujao kwa Yanga ni dhidi ya Tabora United ambapo watakuwa ugenini Desemba 23 kikosi cha Yanga kimeanza safari kuwafuata Tabora United miongoni mwa wachezaji waliopo kwenye msafara ni Pacome, Skudu Makudubela, Farid Mussa.