MECKY Maxime, Kocha Mkuu wa Kagera Sugar amesema kuwa wawakilishi wa Tanzania kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga na Simba wanafanya kazi kubwa licha ya kushindwa kupata matokeo mazuri.
Ipo wazi kwamba Yanga na Simba zinaipeperusha bendera ya Tanzania kwenye hatua ya makundi ambapo timu zote zina pointi mbili baada ya kucheza mechi tatu ndani ya dakika 270.
Maxime amesema kuwa jitihada zao zinaonekana kutokana na kuonyesha ushindani kwenye mechi ambazo wanacheza.
“Yanga na Simba wanacheza mashindano ya kimataifa na ratiba zao ni ngumu kwa kuwa wanacheza kila leo jambo ambalo linazidi kuwaimirisha katika mechi ambazo zinafuata tofauti na sisi ambao kukiwa na mapumziko muda mrefu tunakaa bila kucheza.
“Wapo ambao wanasema ugumu wa ratiba unawafanya wasiwe kwenye ubora lakini ukweli ni kwamba timu inapopata nafasi ya kucheza inazidi kuwa imara kwa ajili ya mechi zinazofuata na kuendeleza ubora wake,” .