WAKIWA kwenye maandalizi ya mwisho kuwakabili wapinzani wao Medeama FC ya Ghana, Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi ametoa maagizo mazito kwa wachezaji wake wote kuanzia kwenye safu ya ushambuliaji na ulinzi.
Ipo wazi kuwa baada ya kucheza mechi tatu katika hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika, safu ya ushambuliaji ya Yanga ilitupia mabao mawili huku safu ya ulinzi ikiruhusu kufungwa mabao matano.
Akizungumza na Spoti Xtra, Gamondi alisema kuwa kuna umuhimu mkubwa kila sekta kutimiza majukumu kwa ushirikiano ikiwa ni upande wa ushambuliaji kutumia nafasi watakazopata kufunga na upande wa ulinzi kuzuia kutokufungwa.
“Ni hatua ngumu tuliyopo na hata ushindani ni mkubwa. Kinachotakiwa kwa wachezaji wote ni kuongeza ushirikiano na umakini. Pale washambuliaji wakipata nafasi na kufunga bao ni jukumu la timu nzima kushirikiana kuona namna gani tutazuia kuruhusu kufungwa.
“Ukitaka kushinda ni lazima ufunge na kuzuia kufungwa, ikitokea ukafunga na kufungwa inaongeza ugumu kufikia malengo. Ninawaamini wachezaji wote wanajituma na kutafuta ushindi kwa juhudi hivyo kwa mechi zinazofuata itakuwa hivyo,” alisema Gamondi.
Desemba 20 Yanga inatarajiwa kuwa Uwanja wa Mkapa kusaka pointi tatu dhidi ya Medeama mchezo uliopita wakiwa ugenini waligawana pointi mojamoja kwa kufungana bao 1-1.
Kwenye kundi D Yanga ina pointi mbili ikiwa nafasi ya nne huku vinara wakiwa ni Al Ahly wenye pointi 5.