WAKIWA na kibarua cha kusaka ushindi kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika, dhidi ya Wydad Casablanca leo Jumanne, kocha mkuu wa Simba, Abdelhack Benchikha amefumua kikosi na kubainisha mambo saba yatakayoipa ushindi timu hiyo.
Ipo wazi kwamba Wydad Casablanca nao hesabu zao kubwa ni kupata ushindi hivyo zitakuwa ni dakika 90 za kazi kubwa, kwa wababe hawa kusaka ushindi Uwanja wa Mkapa mchezo utakaochezwa saa 10 jioni.
Benchikha amesema mambo muhimu ambayo yatawapa ushindi ikiwa ni pamoja na kujiamini kwa wachezaji, kucheza wakiwa nyumbani pamoja na wachezaji kuwa na nguvu ya kujituma kutokana na uwezo uliopo kwenye juhudi, ari na ushirikiano.
“Mchezo wetu dhidi ya Wydad Casablanca ni mgumu kwa kuwa hautakuwa rahisi lakini kuna mengi tumefanyia kazi ikiwa ni pamoja na kuongezeka hali ya kujiamini kwa wachezaji hilo tunajivunia, kwakuwa kila mchezaji anaonyesha ubora sehemu ya mazoezi na tunatarajia itakuwa hivyo kwenye mechi.
“Ikumbukwe kwamba tutakuwa nyumbani, hili linaongeza nguvu kwa wachezaji kucheza kwa kujiamini wakiwa na nguvu kubwa ya kutafuta ushindi. Jambo lingine wachezaji wanajituma wakiwa na ari na kuonesha uwezo mkubwa bila kusahau ushirikiano uliopo katika kikosi,” alisema Benchikha.
Jembe la kazi Wydad kukosekana
Nahodha wa Wydad Casablanca, Yahya Jabrane anatarajiwa kutokuwa kwenye mpango kazi wa kikosi cha timu hiyo kutokana na kutumikia adhabu ya kadi tatu za njano kama ilivyo kwa nyota wa Simba, Sadio Kanoute.
Ikumbukwe kwamba Jabrane alionyeshwa kadi hiyo kwenye mchezo dhidi ya Simba dakika ya 62 baada ya kumchezea madhambi kiungo wa Simba, Clatous Chama na kuonyeshwa kadi ya njano ambayo ilikuwa ni ya tatu kwake.
Kikosi cha ushindi
Kutokana na kukosekana kwa Kanoute kikosi kazi cha ushindi kinatarajiwa kuwa na mabadiliko ambapo kinatarajiwa kupangwa namna hii: Ayoub Lakred, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Che Malone, Henock Inonga, Fabrince Ngoma, Kibu Dennis, Mzamiru Yassin, Jean Baleke, Clatous Chama na Willy Onana.