YANGA MATUMAINI MAKUBWA KIMATAIFA

UONGOZI wa Yanga umebainisha kuwa bado una nafasi ya kufanikisha malengo yao licha ya kuanza kwa kusasua kwenye mechi za mbili za hatua ya makundi, Ligi ya Mabingwa Afrika.

Baada ya kukomba dakika 180 kibindoni ni pointi moja ilivunwa kutokana na sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya Al Ahly, mchezo uliochezwa Uwanja wa Mkapa.

Kituo kinachofuata kwa Yanga ni Desemba 8 dhidi ya Medeama ya Ghana mchezo ambao Yanga watakuwa ugenini na alfajiri ya Desemba 5 msafara wa Yanga ulianza safari kuwafuata wapinzani wao na Desemba 6 waliwasili Ghana.

 Ally Kamwe, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Yanga amesema kuwa wanamatumaini ya kufanya vizuri kwenye mechi zao zilizobaki.

“Tupo kwenye mashindano makubwa na timu yetu ni kubwa Afrika. Tuna matumaini ya kufanya vizuri kwenye mechi zetu licha ya matokeo ambayo tumeyapata kwenye mechi zilizopita.

“Ukweli ni kwamba kila mchezo kwetu ni muhimu kupata matokeo chanya, wachezaji wanatambua umuhimu wa mechi zetu hivyo tunaamini kazi ya mapambano itakuwa kubwa,” amesema Kamwe.

Yanga leo inatupa kete yake ya pili kwenye Ligi ya mabingwa Afrika dhidi ya Medeama mchezo unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa ndani ya dakika 90 chini ya Kocha Mkuu, Miguel Gamondi.

Miongoni mwa wachezaji waliopo Ghana ni pamoja na Aziz KI, Khalid Aucho, Kennedy Musonda.