ZIMETUNGULIWA ZAIDI YA MABAO 10 BONGO

KUFAHAMU ukweli kisha ukaongopa sio utani hiyo inaumiza, muhimu kutibu tatizo lilipo kuwa bora kwenye mechi za ushindani, hivyo tu basi.

Kwenye mwendo wa data tunakuja na timu ambazo zimeokota mabao zaidi ya 10 kwenye mechi ambazo walishuka uwanjani namna hii:-

Mtibwa Sugar

Uwanja wa Manungu huu wanautumia kwa mechi za nyumbani wakiwa na ngome yao pale Morogoro. Mwendo wao ni wa kuasuasua ikiwa tayari ilishampa mkono wa asante Habib Kondo.

Ipo chini ya Kocha Mkuu, Zuber Katwila, Mtibwa Sugar baada ya kucheza mechi 11 ni namba moja kwa timu zilizookota mabao mengi kwenye nyavu ambayo ni mabao 23.

Safu ya ushambuliaji ilipata nafasi ya kufunga mabao 11 ikiwa na pointi 5 kibindoni ipo nafasi ya 16.

Tanzania Prisons

Ilianza mikononi mwa Felix Minziro ambaye alipewa mkono wa asante. Ni Tanzania Prisons baada ya kucheza mechi 11 ilishuhudia mabao ya kufungwa 16.

Ile safu ya ushambuliaji ilitupia mabao 10 ilikusanya pointi 10 ikiwa nafasi ya 13.

Ihefu

Kutoka Mbeya wanatumia Uwanja wa Highland Estate. Ihefu baada ya kucheza mechi 11 ilishuhudia ikiokota mabao ya kufungwa 15 huku ile safu ya ushambuliaji ikitupia mabao 8 pointi 9 ikiwa nafasi 14.

JKT Tanzania

JKT Tanzania ipo nafasi ya 6 ule ukuta wao uliruhusu mabao ya kufunga 11, mabao ya kufungwa 15 kibindoni ni pointi 16.

Singida Fountain Gate

Singida Fountain Gate ipo nafasi ya nne mechi za kucheza 12. Ile safu ya ulinzi ilishuhudia mabao ya kufungwa 15  mabao ya kufunga 17 pointi 19.

KMC

Wakusanya mapato KMC baada ya kucheza mechi 11 ilifungwa mabao 14. Ile safu ya ushambuliaji ilitupia mabao ya kufunga 13. Kibindoni ni pointi 19 ikiwa nafasi ya 5.

Geita Gold

Geita Gold baada ya kucheza mechi 12 iligotea nafasi 11 na mabao ya kufungwa 14. Ile safu ya ushambuliaji ni mabao ya kufunga 8 na pointi 13 kibindoni.

Mashujaa FC

Mashujaa FC ya Kigoma mwendo wake umeifanya iwe nafasi ya 15 huku  ikifungwa mabao 12 na ile safu ya ushambuliaji ikitupia mabao 7 pointi 8.

Dodoma Jiji

Wakulima wa zabibu, Dodoma Jiji ilifungwa mabao 12 ikiwa nafasi ya 7 safu ya ushambuliaji ilifunga mabao 11 pointi 15.

Coastal Union

Coastal Union ya Tanga baada ya mechi 12 ilifungwa mabao 11 ilifunga mabao 9 pointi 13.

Simba

Ni namba moja kwa timu zilizo tatu bora kufungwa mabao mengi. Baada ya kucheza mechi 8 Simba  ilifungwa mabao 11 nafasi ya tatu pointi 19 ilifunga mabao 18.