>

SINGIDA FOUNTAIN GATE KUKIWASHA NA WAJEDA

HELO Desemba Mosi Ligi Kuu Tanzania Bara inaendelea kutimua vumbi ambapo leo Desemba Mosi, Uwanja wa Liti dakika 90 za jasho zinatarajiwa kuwa kwa wababe watakaokuwa wakisaka pointi tatu.

Singida Fountan Gate iliyotoka kushinda mabao 2-1 dhidi ya Coastal Union itakabiliana na Wajeda, JKT Tanzania kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza.

Hussein Masanza, Ofisa Habari wa Singida Fountain Gate amesema kuwa wapo tayari kwa mchezo wa leo dhidi ya JKT Tanzania na wanahitaji kuchukua alama tatu.

Ikumbukwe kwamba kwenye mchezouliopita dhidi ya Coastal Union nyota wao Meddie Kagere alifungua akaunti ya mabao ndani ya ligi.

Massanza amesema:”Tunatambua ushindani ni mkubwa na wapinzani wetu JKT Tanzania sio timu ya kubeza ila tunahitaji kuendelea pale ambapo tuliishia.

“Ushindi wetu mchezo uliopita dhidi ya Coastal Union umeongeza nguvu kwetu hivyo tutakabiliana na wapinzani wetu kwa tahadhari kupata pointi tatu,” amesema.

Miongoni mwa nyota ambao wapo kwenye kikosi cha Singida Fountain Gate ni kipa namba moja Beno Kakolanya, Meddie Kagere, Deus Kaseke, Gadiel Michael, Bruno Gomes, Dickson Ambundo.