Home Sports DULLAH MBABE KAPIGWA TENA NA UBABE WAKE

DULLAH MBABE KAPIGWA TENA NA UBABE WAKE

BONDIA wa ngumi za kulipwa nchini, Abdallah Pazi ‘Dullah Mbabe ameendelea kuwa mteja wa mpinzani wake Tshimanga Katompa raia wa DR Congo kufuatia kukubali kichapo kwa mara ya pili mfululizo.

Katika pambano hilo ambalo limepigwa juzi usiku kwenye Ukumbi wa Hoteli ya Mount Meru jijini Arusha chini ya promosheni ya Red in Lady Promotion inayoongozwa na Mbunge wa Viti Maalum, Sophia Mwakagenda.

Mbabe alipanda ulingoni katika pambano hilo akiwa nakumbumbuku mbaya za kupoteza kwa pointi mwaka juzi dhidi ya bondia huyo kabla ya juzi Jumamosi kupoteza  tena kwa mara ya pili  kwa pointi katika pambano hilo ambalo Mbabe alionyesha ubabe wake katika raundi tatu pekee za mwanzo kabla ya mambo kumuendea mrama.

Mbabe alianza pambano hilo la raundi kumi katika uzani wa middle kwa kasi kubwa huku akimpa wakati mgumu mpinzani wake Katompa ambaye alikuja kubadilika baada ya raundi tatu kufuatia kubadilisha mguu kutoka wakulia na kucheza na mguu wa kushoto.

Hali hiyo ilipelekea kumpa wakati mgumu Mbabe ambaye alidhamiria kulipiza kisasi kutokana na kuishiwa nguvu huku muda mwingi akionekana kuegemea kwenye kamba ili kukwepa KO kabla ya kutangazwa matokeo yaliopelekea Dullaha Mbabe kupoteza kwa majaji wote watatu.

Baada ya pambano hilo, Dullah Mbabe alisema kuwa kila Mtanzania ameona namna alivyomthibiti Katompa lakini ameshangaa kuona hakuweza kupewa ushindi kufuatia madai yake kutokubalika na majaji wa mchezo huo nchini kauli iliyoungwa mkono na swahiba wake Ibrahim Class ambaye alikuwa akilia kwa uchungu.

Lakini kwa upande wa mabondia wengine, Sara Alex amemtwanga kwa pointi Tatiana Ezekiel sawa na Shaban Ndaro ambaye alimshinda kwa pointi Salehe Mkalekwa huku Alibaba Tarimo akiendeleza utemi wake kwa kumbonda Karage Suba.

Mtanzania, Loren Japhet yeye amefanikiwa kupeperusha bendera ya Tanzania vyema kwa kuweza kumchapa kwa pointi Rilwan Lawal wa Nigeria wakati Paul Kamata na Jacob Maganga wakiambulia sare huku Leila Macho akimtwanga kwa pointi Chiku Said lakini Shaban Kaoneka akimparua kwa pointi Kasim Pesa.

Previous articleBOSI SIMBA AMEFUNGUKA MWENDO WA TIMU NA UGUMU ULIOPO
Next articleYANGA YASAINI DILI NONO KUELEKEA KUWAKABILI WAARABU