UONGOZI wa Simba umeweka wazi kuwa utadhihirisha ukubwa wao kwa kupata ushindi kwenye mchezo wa Kariakoo Dabi dhidi ya Yanga unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mkapa.
Ni Kariakoo Dabi inayotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa ndani ya dakika 90 kwa timu zote kuwania kupata pointi tatu muhimu.
Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally ameweka wazi kuwa wanatambua ushindani utakuwa mkubwa na wapo tayari kwa ajili ya kupata matokeo kwenye mchezo huo.
“Mchezo dhidi ya Yanga utachezwa siku ya Jumapili Novemba 5, 2023 saa 11:00 jioni katika Uwanja wa Mkapa. Ni mechi kubwa kwetu, ni mechi ambayo inakwenda kuonyesha ubora halisi ya mpira wa Tanzania na ushindi wake unaleta tabasamu kwa mashabiki wa timu husika na kupoteza kunaacha majonzi.”
“Ni mechi ambayo tunakwenda kuendeleza ubabe kwa watani zetu. Ili tujiridhishe kwamba msimu huu tutafanya vizuri ni kupata ushindi katika mchezo huo. Tunataka tuchukue ubingwa mapema sana, katika hili tunawashukuru Ihefu kwa kutusaidia kazi na sisi tunataka kuendeleza kuweka tofauti ya alama na Yanga,” .