MARA baada ya kuondolewa na Al Ahly ya nchini Misri katika michuano ya African Football League (AFL), Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amesema kuwa sasa hivi akili zao wanazielekeza katika Ligi Kuu Bara na kikubwa kurejea kileleni.
Kauli hiyo huenda ikawa kijembe kwa wapinzani wao, Yanga ambao wanaongoza ligi wakiwa na pointi 15 sawa na Simba ambao wapo nyuma mchezo mmoja.
Simba wenyewe wanatarajiwa kujitupa kwenye Uwanja wa Mkapa Jijini Dar es Salaam kesho Jumamosi kuvaana dhidi ya Ihefu FC katika mchezo wa ligi.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Ahmed alisema kuwa hasira zote za kuondolewa katika African Footabll League, wanazihamishia katika ligi kwa lengo la kubeba ubingwa huo.
Ahmed aliongeza kuwa kwa kuanza wataanza na mchezo ujao wa ligi dhidi ya Ihefu, ambao wamepanga kuwashushia kipigo kizito kwa lengo la kuwaondoa kileleni Yanga.
Aliongeza kuwa wapinzani wao Yanga wamekaa kwa muda katika nafasi hiyo, wakati wao wakiwa wanacheza michuano hiyo mipya ya AFL.
“Rasmi tumerejea katika ligi, kwa kuanza tunatarajiwa kuanza na Ihefu Jumamosi (kesho) hii tutakapokutana kwenye Uwanja wa Mkapa katika mchezo wa ligi.
“Tumepanga kurejea kwa kishindo katika ligi, kwa kutoa dozi kwa kila timu tutakayokutana nayo, ninafahamu haitakuwa rahisi kupata ushindi huo, lakini wachezaji wetu watahakikisha wanapambana.
“Ihefu hawawezi kutusumbua, wapo wanaowasumbua lakini sio wao, tumepanga kuonyesha ukubwa wetu Simba katika ligi,” alisema Ahmed.