JOB MTU WA KAZIKAZI YANGA

DICKSON Job beki bora wa msimu wa 2022/23 bado anaonyesha thamani yake uwanjani kuwa ni chuma cha kazi kutokana na kuwa ni chaguo la kwanza la Miguel Gamondi.

Job anayekipiga ndani ya kikosi cha Yanga ni shuhuda timu hiyo ikikomba pointi tatu mazima dhidi ya Azam FC kwenye Mzizima Dabi kwa mabao ya Aziz KI ambaye alifunga hat trick kwenye mchezo huo mkubwa.

Rekodi zinaonyesha kuwa Yanga ikiwa imecheza mechi sita ambazo ni dakika 540, mwamba Job kazikomba zote mazima kutokana na kuwa na mwendelezo mzuri kwenye mechi anazopewa nafasi.

Ikumbukwe kwamba safu ya ushambuliaji ya Yanga imetupia mabao 18 kwenye mechi sita ikiwa na wastani wa kufunga bao moja kila baada ya dakika 30, mtupiaji wa bao la kwanza msimu wa 2023/24 ni Job aliyefanya kazi hiyo kwenye mchezo wa ligi dhidi ya KMC, Uwanja wa Azam Complex.

Safu ya ulinzi ya Yanga imeokota jumla ya mabao manne ilikuwa dhidi ya Ihefu na Azam FC ilipotunguliwa mabao mawilimawili na kipa langoni alikuwa ni Djigui Diarra.