HABARI njema kwa mashabiki wa Yanga, kuwa beki wa kazi wa timu hiyo raia wa Ivory Coast, Yao Kouassi Attohoula, amepona majeraha na yupo tayari kwa mchezo ujao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Singida Fountain Gate utakaochezwa kesho Ijumaa.
Mbali na Yao, pia kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Farid Mussa, naye amerejea kikosini baada ya kukosekana kwa takribani mechi nne.
Nyota hao walikosekana katika mchezo uliopita wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam FC uliochezwa Uwanja wa Mkapa, Dar, ambao Yanga ilishinda 3-2.
Akizungumza na Spoti Xtra, Kocha Mkuu wa Yanga, Muargentina, Miguel Gamondi, alisema katika mchezo uliopita aliwakosa wachezaji hao ambao wanatarajiwa kuwepo dhidi ya Singida.
Gamondi alisema wachezaji hao wapo fiti na tayari kwa ajili ya kuipambania Yanga, kwa kuanzia mchezo ujao wa ligi dhidi ya Singida, huku akiongeza kwamba, kurejea kwao kutampa wigo mpana wa kupanga kikosi.
“Katika mchezo uliopita wa ligi dhidi ya Azam, niliwakosa wachezaji wawili muhimu kutokana na majeraha, lakini niwaondoe hofu mashabiki kuwa wachezaji hao wote wamepona na wapo fiti kwa kucheza dhidi ya Singida.
“Mchezo dhidi ya Azam, nililazimika kumtumia Job (Dickson) kucheza nafasi ya Yao, lakini katika mchezo ujao dhidi ya Singida atakuwepo.
“Nimpongeze Job kwa kucheza vizuri nafasi hiyo ya beki wa kulia, alicheza kwa kufuata maelekezo yangu ambayo nilimpa kwanza kujilinda na kuanzisha mashambulizi,” alisema Gamondi.