BEKI wa pembeni tegemeo wa Yanga, Muivory Coast, Yao Kouassi ameandaliwa kwa kupewa mbinu za kufunga kila anapofika ndani na nje 18 ya goli la wapinzani.
Yao amekuwa tegemeo kubwa katika kikosi cha Yanga katika kuanzisha mashambulizi huku akikaba katika goli lake.
Nyota huyo hadi hivi sasa amefunga amepiga asisti tatu huku akifunga bao moja pekee katika michezo sita ya Ligi Kuu Bara.
Mmoja wa Mabosi wa Benchi Ufundi amesema Kocha Mkuu wa Yanga Muargentina Miguele Gamondi wiki iliyopita aliwapa program mabeki wote pembeni mbinu za kufunga mabao.
Bosi huyo alisema kuwa kikubwa anataka kuona mabeki hao wakifunga na kutengeneza nafasi za mabao kutokana na uwezo mkubwa waliokuwa nao nyota hao Joyce Lomalisa, Kibwana Shomari, Nickson Kibabage na Yao mwenyewe.
“Kama unavyofahamu kuwa timu inatengeneza mabao kupitia pembeni, hivyo kocha ameona ni bora akawaongezea baadhi ya mbinu za kufunga mabao sio tu kutengeneza mabao pekee.
“Hivyo kocha ameona ni bora akawaongezea ufundi mabeki hao akiwemo Yao ambaye mara kadhaa amekuwa akifika ndani ya 18 ya goli la wapinzani na kukosa utulivu wa kufunga mabao,”.
Gamondi alizungumzia hilo kwa kusema kuwa “Katika timu yangu ninataka kumuona mchezaji akifunga mabao, sitaki awepo mchezaji mmoja tegemeo katika kufunga mabao.
Mchezo ujao kwa Yanga ambao ni vinara wa ligi ni dhidi ya Singida Fountain Gate Oktoba 27, Uwanja wa Mkapa.