KAZI IPO KWA WACHEZAJI WA SIMBA KIMATAIFA

MAJIBU ya nani atakuwa mshindi atakayesonga hatua ya nusu fainali kwenye mashindano mapya ya African Football League kati ya wawakilishi wa Tanzania, Simba dhidi ya Al Ahly ya Misri yanasubiriwa leo.

Ukweli ni kwamba mchezo wa leo una maana kubwa kwa Simba kuandika rekodi mpya ambayo itabaki kwenye kumbukumbu za muda wote. Ni mchezo mgumu na mkubwa utakaochezwa na wakubwa.

Makosa ambayo yalitokeza kwenye mechi zilizopita ni muda wa kuyafanyia kazi ili kupata ushindi. Itakuwa kazi ngumu kwa wachezaji kuonyesha ukomavu wao ugenini.

Fursa mpya na kubwa kwa wachezaji wote kuutangazia ulimwengu kuwa kuna timu inaitwa Simba kutoka Tanzania. Wachezaji watakuwa sokoni kukuza majina yao yatakayowapa nafasi ya kutoka nje ya Bongo kwa wakati mwingine.

Ipo wazi kuwa kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Mkapa ngoma ilikamilika kwa wababe hao wote kutoshana nguvu hivyo leo ni mwisho wa ubishi.

Kazi inaweza kuishia Uwanja wa Mkapa ikiwa safu ya ushambuliaji, viungo na mabeki hawatakuwa na ushirikiano kwenye kutimiza majukumu yao kwa wakati.

Al Ahly huwa wanakuwa tofauti wakiwa nyumbani hilo wanalitambua Simba kwa kuwa katika mechi za kimataifa hivi karibuni hawakupata nafasi ya kushinda kwenye mechi walizokutana.

Nafasi nyingine ya kupambana na kushirikiana kufanyia kazi makosa ili hatua ya robo fainali isiwe ni wimbo wa Simba kwenye mafanikio yao kila mara.