MIGUEL Gamondi, Kocha Mkuu wa Yanga ameweka wazi kuwa wachezaji wake wote wapo tayari kwa ajili ya mchezo dhidi ya AzamFC.
Leo ni Mzizima Dabi inatarajjiwa kupigwa Uwanja wa Mkapa, Oktoba 23 kwa wababe wawili kusaka pointi tatu.
Miongoni mwa silaha ambazo zipo tayari kuikabili Azam FC ni Skudu Makudubela, Farid Mussa, Khalid Aucho, Jesus Moloko, Sure Boy, Jonas Mkude.
Itakuwa ni mara ya pili kwa vigogo hawa Yanga na Azam FC kukutana uwanjani kwenye mechi za ushindani.
Mara ya kwanza vigogo hao kukutana ilikuwa kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii, ubao wa Uwanja wa Mkwakwani ulisoma Yanga 2-0 Azam FC.
Gamondi amesema kuwa wanatambua wapinzani wao ni wazuri jambo linalowafanya wajiandae kwa umakini kupata matokeo mazuri.
“Wachezaji wapo tayari na tutaingia kwenye mchezo wetu dhidi ya Azam FC tukitambua hautakuwa mwepesi na kikubwa ni kupata ushindi kwenye mchezo wetu.
“Kwenye uwanja wa mazoezi tunafanyia kazi makosa ambayo tulifanya kwenye mchezo uliopita. Kufanya kazi kwenye mechi zinazofuata kunatupa muda wa kuwa bora kuwakabili wapinzani wetu na kikubwa ni kuona tunapata pointi tatu,” amesema Gamondi.