MRITHI wa mikoba ya Fiston Mayele ndani ya kikosi cha Yanga, Kennedy Musonda anapambania kombe kutokana na kuendelea kujitafuta kwenye kufunga ndani ya ligi.
Ikumbukwe kwamba Mayele aliyesepa ndani ya kikosi cha Yanga msimu wa 2022/23 alikuwa ni namba moja kwa utupiaji alipotupia mabao 17 kibindoni na kutwaa tuzo ya ufungaji bora.
Kwa sasa yupo zake ndani ya Klabu ya Pyramids ya Misri na mbeba mikoba wake kikosini hapo ni Mzambia Kennedy Musonda.
Musonda anapambania mambo mawili ndani ya Yanga inayonolewa na Kocha Mkuu, Miguel Gamondi jambo la kwanza ni kuwa chaguo la kwanza kwenye kikosi na la pili ni kufunga mabao mengi akiwa katika majukumu yake.
Ni bao moja kafunga kwenye ligi ilikuwa dhidi ya JKT Tanzania mchezo uliochezwa Uwanja wa Azam Complex kwenye anga la kimataifa katupia mabao mawili ilikuwa dhidi ya ASAS FC na Al Merrikh kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kwenye ligi katika mechi tano zenye dakika 450 kapata zali ya kukomba dakika 137 kwenye mechi tatu ambazo alipata nafasi ya kucheza chini ya Miguel Gamondi.