ZIMEBAKI siku tatu kabla ya Mzizima Dabi kupigwa ndani ya Uwanja wa Azam Complex, mastaa wa Azam FC ikiwa ni pamoja na Prince Dube, James Akamiko, Idd Suleiman, (Nado) wanapewa mbinu kuikabili Yanga.
Mastaa hao wapo chini ya Kocha Mkuu, Yusuph Dabo aliyetoka kukiongoza kikosi kusepa na pointi tatu ugenini dhidi ya Coastal Union, kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Mkwakwani.
Kwenye mchezo huo bao la ushindi kwa Azam FC lilifungwa na Feisal Salum mwenye mabao manne ndani ya ligi.
Timu zote mbili zinakwenda kukutana zikiwa na uwiano sawa kwenye orodha ya mabao ya kufungwa ambayo ni mawili, tofauti Azam FC kipa Idrissu Abdulai alitunguliwa bao mojamoja kwenye mechi mbili tofauti huku Djigui Diarra akitunguliwa mabao yote mawili mchezo mmoja dhidi ya Ihefu.
Ni Yanga pekee ina hasira ya kupoteza pointi tatu mazima dhidi ya Ihefu ikikusanya jumla ya pointi 12 kwenye mechi tano huku Azam FC ikiwa haijapoteza mchezo na kibindoni ina pointi 13.
Dabo ameweka wazi kuwa kila baada ya mchezo wanafanyia kazi makosa ili kuwa tayari kwa dakika 90 zinazofuata kwenye mechi zao zote.
“Kila baada ya mchezo tunaanza maandalizi ya kupata pointi tatu kwa mechi inayofuata. Wachezaji wanajituma na makosa yanayoonekana kwenye mechi husika tunafanyia kazi kwenye uwanja wa mazoezi,”.
Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa Azam Complex, Oktoba 23.