UONGOZI wa Simba umeweka wazi kuwa uwepo wa wachezaji wanaofanya vizuri kwenye kikosi hicho eneo la uwanja wa mazoezi ni nguvu kubwa kuelekea mchezo wao dhidi ya Al Ahly unaotarajiwa kuchezwa Oktoba 20.
Kikosi cha Simba kinachonolewa na Kocha Mkuu, Roberto Oliveira kinaendelea na mazoezi kuelekea mchezo wa African Football League utakaochezwa Uwanja wa Mkapa.
Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano, Simba Ahmed Ally amesema kuwa kuna wachezaji ambao wanazidi kuimarika na uwezo wao utaonekana Uwanja wa Mkapa.
“Kuna mtaalamu wa pasi zenye uhakika kiungo Fabrince Ngoma ana hatari huyo yule ambaye alionekana kwenye ligi atakuwa tofauti kabisa Oktoba 20 dhidi ya Al Ahly.
“Sio Ngoma pekee yupo Luis Miquissone wengi wanambeza basi atawaonyesha ubora wake kwa vitendo. Kwenye ulinzi tupo na ukuta imara Che Malone huyu kazi yake inaonekana usisahau kuhusu Shomari Kapombe na Mohamed Hussein ni watu wa kazi haswa.
“Kikubwa mashabiki wajitokeze kwa wingi kushuhudia kwa vitendo hizi burudani kwani ambacho kinatafutwa ni matokeo na huu mchezo tunaamini utakuwa na ushindani sisi tupo tayari,” amesema Ally.