UONGOZI wa Klabu ya Yanga leo Oktoba 9,2023 umeingia makubaliano na Kampuni ya Bima, NIC kwa ajili ya kudhamini tuzo za mchezaji bora wa mwezi.
Hayo ni makubaliano ya muda wa miaka mitatu ambapo ni milioni 900 zitapatikana kwa muda wa miaka mitatu.
Akizungumza kuhusu hilo Rais wa Klabu ya Yanga, Injinia Hersi Said amesema kuwa hiyo ni fursa kwao itakayotumiwa vema na wachezaji kuendelea kutimiza majukumu yao uwanjani huku wakiendeleza mahisiano mazuri ya kibiashara na NIC.
“Makubaliano haya ya kibiashara kimsingi yanakwenda kunufaisha pande zote. Yanga inakwenda kupata kiasi cha shilingi 900m kwa kipindi cha miaka mitatu. NIC nao wanapata fursa ya biashara yao kutangazwa kwa ukubwa.
“Tunaelewa kwanini wamechagua kufanya kazi na sisi. Tuna wachezaji bora zaidi ambao huwezi kuwapata kwenye klabu nyingine. Wachezaji hawa wana ushawishi mkubwa nje na ndani ya uwanja. Ushawishi wao ni chachu ya kutangaza biashara,” amesema Hersi.
Elihuruma Doriye, Mtendaji Mkuu NIC amesema: “Historia imeandikwa baada ya taasisi mbili zenye chapa ya kihistoria kwa Tanzania kuingia makubaliano ya kibiashara kwa miaka mitatu.
“Huwezi kuzungumzia BIMA bila kuitaja NIC, na katika soka Yanga ni nembo ya soka kwa Tanzania akiwa bingwa wa kihistoria. Tunayo furaha kubwa kupata fursa ya kufanya biashara na taasisi kubwa kama hii. Kwa upande wetu NIC imepewa hadhi ya kuaminika,”.
Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe amesema: “Tunafurahi sana kuingia mkataba na NIC kwa sababu kutakuwa na ushindani mkubwa kwa wachezaji wetu. Hamasa itakuwa kubwa kutoka kwa mashabiki. Bila shaka michezo yetu watakao trend mitandaoni baada ya mechi ni wachezaji tu na sio mtu mwingine,” .