GAMONDI: TUTAWAFURAHISHA CAF NA KUPATA USHINDI

MIGUEL Gamondi, Kocha Mkuu wa Yanga amesema kuwa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuwatambua wapinzani wao katika hatua ya makundi watacheza kwa kutafuta ushindi na kuwafurahisha mashabiki.

Makundi CAF yalipangwa Oktoba 6 Afrika Kusini na Yanga ikipangwa kundi D ikiwa na timu za Al Ahly ambao ni mabingwa watetezi, CR Belouizdad ya Algeria, Medeama ya Ghana.

Hii ni historia nyingine Yanga inakwenda kuandika baada ya kuyeyusha miaka 25 bila kushiriki hatua ya makundi kwenye mashindano haya makubwa.

Kocha huyo amesema: “Tunatambua wapinzani wetu katika Ligi ya Mabingwa Afrika ni imara nasi tutafanya kazi kutafuta ushindi. Ni kazi kubwa kwenye mechi za kimataifa hilo tunalitambua lakini tutacheza kwa umakini kupata ushindi na kuwafurahisha.

“Wachezaji wapo tayari kuona tunapata ushindi na makosa kwenye mechi zilizopita tunafanyia kazi ili kuwa bora na imara zaidi.

“Mashabiki wakijitokeza kwa wingi uwanjani inatuongezea nguvu ya kupata matokeo. Imani yetu ni kuona tunakuwa na mwendo mzuri kwenye mechi ambazo tunacheza,”.