SIMBA MIKONONI MWA SINGINDA FG NA MSAKO WA REKODI

KOCHA Mkuu wa Simba, Roberto Oliveira amesema kuwa wanahitaji kuendelea na rekodi zao za kupata matokeo kwenye mechi za ligi ikiwa ni pamoja na mchezo dhidi ya Singida Fountain Gate.

Leo Simba inatarajiwa kushuka kwenye msako wa pointi tatu dhidi ya Singida Fountain Gate kwenye mchezo unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Liti.

Huu utakuwa ni mchezo wa 16 kwa Oliveira kwenye ligi kuongoza kikosi cha Simba ambapo kwenye mechi 15 zilizopita ni 13 alishinda na mbili aliambulia sare.

Kocha huyo amesema: “Tunahitaji kupata matokeo mazuri kwenye mchezo wetu dhidi ya Singida Fountain Gate. Rekodi yetu ya kucheza bila kupoteza hiyo ni muhimu kuendelea na tunajua kuwa utakuwa mchezo mgumu.

“Kikubwa ni kutambua kwamba wachezaji wapo tayari na maandalizi ambayo tumefanya yanatupa nguvu ya kupata matokeo mazuri kwenye mchezo wetu,” .

Mchezo uliopita kwa Simba ugenini ilishuhudia ubao wa Uwanja wa Sokoine ukisoma Tanzania Prisons 1-3 Simba.