KILA mmoja anatambua kwamba pazia la Ligi Kuu Bara linakwenda kufunguliwa leo ambapo kuna mechi zitakazoanza kuchezwa katika viwanja tofauti.
Yanga ambao ni mabingwa watetezi hawa kete yao ya kwanza itakuwa dhidi ya KMC wote ni watoto wa mjini.
Simba iliyogotea nafasi ya pili kibarua chake ni dhidi ya Mtibwa Sugar itakuwa ugenini kwenye mchezo wa ufunguzi.
Azam FC ambao kwenye Ngao ya Jamii ilitoka kuwakanda Singida Fountain Gate itakuwa nyumbani kwenye mchezo wao wa ufunguzi na sasa ligi inaanza upya msimu wa 2023/24.
Yote haya yanakuja baada ya mashindano ya Ngao ya Jamii 2023 kukamilika ambapo yalifanyika pale Mkwakwani, Tanga.
Mashabiki wameona namna ilivyokuwa kwa kila timu kupambana kupata matokeo na mwisho mshindi amepatikana baada ya kuwa na matumizi ya nguvu pamoja na akili.
Tumeona wachezaji wapo waliopewa maumivu na wachezaji wenzao uwanjani kwenye kupambana na kusababisha wakwame kuonekana kwenye mechi nyingine.
Kwa sasa benchi la ufundi bado linafikiria wale ambao watapewa majukumu yao kutokana na wachezaji hao kutokuwa fiti hili ni sehemu ambalo linapaswa kufanyiwa kazi.
Ipo wazi kwamba mchezo wa mpira una matumizi mengi ya nguvu lakini ni muhimu kila mchezaji kuwa makini kwa ajili ya usalama ya mchezaji mwenzake.
Kuanza kwa ligi ni ishara kwamba nguvu zinakwenda kutumika lakini ni lazima zitumike kwa umakini bila kuumizana kwa kuwa kazi ya mpira sio vita.
Wale ambao walipata maumivu wakirejea hakuna umuhimu wa kuleta visasi kazi yao iwe ni kusaka ushindi kwenye mechi ambazo watapewa majukumu ya kufanya.
Ni msimu mpya tunatarajia yale ambayo yalikuwa ni mapungufu kwa msimu uliopita yanafanyiwa kazi hilo litakuwa na umuhimu pia kwa afya ya soka letu.
Waamuzi iwe ni haki kwenye mechi zote ambazo mtakuwa kwenye majukumu yenu na wachezaji tendeni haki kwa kucheza kwa umakini.