IWE NI KARIAKOO DABI YA AMANI

KARIAKOO Dabi inatarajiwa kuwa leo Uwanja wa Mkwakwani ambapo hii ni hatua ya fainali Ngao ya Jamii kwa timu zote kusaka ushindi.

Ni Yanga dhidi ya Simba mchezo ambao unasubiriwa kwa shauku kubwa na mashabiki na wachezaji wenyewe kuonyesha uwezo wao uwanjani.

Baada ya maandalizi ya muda pamoja na usajili kuendelea kufanyika wakati uliopo sasa ni kuelekea maandalizi ya Ligi Kuu Bara ambayo ipo njiani.

Kutokana na mwanzo mgumu kwa timu zote kusaka ushindi pamoja na maandalizi basi fainali iwe ni ya haki bila uwepo wa matumizi ya nguvu sehemu isiyotakiwa.

Ipo wazi kwamba wanapokutana mafahari hawa wawili kazi huwa inakuwa ngumu kwa kila mpinzani kupiga hesabu za kupata ushindi.

Jambo la msingi ni kila mmoja kufanya kazi kubwa huku sheria 17 zikifuatwa kwa mchezaji na benchi la ufundi kupambana kupata ushindi.

Ikiwa makosa makubwa yatafanyika kwenye mchezo wa  leo hasara yake ni kubwa ukizingatia kwamba wengi wanakuwa kwenye eneo la tukio.

Mashabiki wengi wanafuatilia pambano hili kutokana na utani wa jadi uliopo pamoja na usajili wa timu hizi mbili zenye ushindani mkubwa.

Kila mmoja ni muhimu kutimiza majukumu yake ndani ya dakika 90 ili kuongeza nguvu ya kupata ushindi na kuwapa furaha mashabiki.

Kwa mashabiki ni muhimu kuwa na utulivu hakuna ambaye anatambua matokeo ya mchezo wa leo bali dakika 90 zitaamua nani atakuwa mshindi.

Waamuzi mtakaopewa majukumu ya kusimamia haki iwe hivyo tu basi zile hadithi za makosa ya kibinadamu zisipewe nafasi.