DODOMA JIJI HAWAPOI, WAJA NA MKWARA HUU

UONGOZI wa Dodoma Jiji umeanza kutamba mapema baada ya ratiba ya Ligi Kuu Bara kutangazwa huku wakitarajia kufungua pazia kwa kusaka pointi tatu dhidi ya Coastal Union ya Tanga.

Mabingwa wa ligi msimu wa 2022/23 ni Yanga waliokuwa wakinolewa na Nasreddine Nabi ambaye hatakuwa ndani ya kikosi hicho kwa msimu wa 2023/24.

Mbali na Nabi kusepa ndani ya Yanga pia mfungaji bora Fiston Mayele naye hatakuwa ndani ya kikosi cha Yanga msimu mpya.

Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa Uwanja wa Jamhuri, Dodoma ambapo walima zabibu hao watakuwe wenyeji dhidi ya Coastal Union inayofundishwa na Mwinyi Zahera.

 Ofisa Habari wa Dodoma Jiji, Moses Mpunga amesema kuwa wanatambua namna walivyojipanga pamoja na utayari wao kwenye mwanzo wa ligi msimu mpya wa 2023/24.

“Iwe jua iwe mvua tumejipanga vizuri kwa ajili ya ligi na furaha kubwa ni kwamba tunaanzia Uwanja wa Jamhuri nyumbani hapo lazima tupate pointi tatu ikishindikana sana labda pointi moja kwani wachezaji wapo tayari na maandalizi makubwa ambayo yamefanyika yanatupa matumaini ya kupata ushindi.

“Kwenye mechi ambazo tunacheza Uwanja wa Jamhuri tumekuwa na bahati ya kupata matokeo. Ratiba namna ilivyopangwa hakuna atakayelaumu kuwa ni ngumu au inabana imepangwa kwa mpangilio mzuri na sisi tunaanza nyumbani Agosti 15 ikiwa ni baada ya kushuhida fainali ya Ngao ya Jamii,” amesema.