UONGOZI wa Dodoma Jiji FC umesema maandalizi yao kwa ujumla na jinsi walivyotumia kipindi cha pre season kuwafua zaidi wachezaji wao kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara wanaimani kubwa ya kumaliza nafasi tano za juu.
Dodoma Jiji wanatambua kwamba walipishana na ubingwa msimu wa 2022/23 ambao ulikwenda Yanga.
Pia katika mchezo wa mzunguko wa pili Uwanja wa Azam Complex ubao ulisoma Yanga 4-2 Dodoma Jiji huku Collins Opare akiwa ni miongoni mwa nyota wa Dodoma Jiji walioifunga Yanga.
Ofisa Habari wa timu hiyo, Moses Mpunga, alisema: “Msimu uliopita uliisha tukiwa nafasi ya 8 tuna uhakika msimu huu tunaotarajia kuuanza tutamaliza tukiwa ndani ya nafasi tano za mwanzo hiyo ndiyo mipango yetu.”
Aidha alieleza utofauti uliopo kwao na baadhi ya timu kwenye suala la kuwapa mkono wa kwaheri ‘Thank You’ wachezaji ambao hawaendelei nao tena.
“Sisi kidogo tupo tofauti pale tunapomalizana na mchezaji wetu basi hatutangazi wazi kwa kuposti kwenye kurasa zetu za mitandao ya kijamii kama wafanyavyo wengine sisi tunaona kufanya hivyo ni kama kumuharibia soko mchezaji huyo bali sisi tunatangaza tu wale tunao wasajili,” alisema Mpunga.
Dodoma jiji FC baada ya ratiba ya ligi kuu kutoka watakuwa wenyeji wa Coastal Union FC Agosti 15, katika Uwanja wa Jamhuri huko jijini Dodoma.