YANGA V AZAM FC KAZI NI NZITO UWANJA WA MKWAKWANI, TANGA

SIO leo tangu msimu wa 2022/23 Yanga na Azam FC wamekuwa wakionyesha upinzani mkubwa uwanjani. Wanafungua kete zao kwenye mchezo wa hatua ya nusu fainali ya kwanza.

Kivumbi leo Uwanja wa Mkwakwani kwa wanaume 22 kusaka ushindi ndani ya uwanja, hapa tunakudondoshea baadhi ya matukio yatakayonogesha mchezo huo:-

Mbinu zinafunguliwa mara ya kwanza

Mbinu za Kocha Mkuu wa Yanga Miguel Angel Gamondi raia wa Argentina zinafunguliwa kwa mara ya kwanza Bongo katika Uwanja wa Mkwakwani Tanga. Unakuwa ni mchezo wake wa kwaza kuiongoza timu hiyo baada ya kupokea mikoba ya Nasreddine Nabi katika mechi za ushindani.

Mbali na majalada ya Gamondi kufunguliwa hata Azam FC ni Msenegal Youssouph Dabo anatarajiwa kukaa kwenye benchi la ufundi mara ya kwanza baada ya kupokea mikoba ya Kali Ongala.

Ngoma inatarajiwa kuchezwa Agosti 9 ikiwa ni hatua ya nusu fainali ya kwanza Ngao ya Jamii na mshindi atakutana na mshindi wa nusu fainali ya pili kati ya Simba dhidi ya Singida Fountain Gate FC itakayochezwa Julai 10 Julai 13 inatarajiwa kuchezwa fainali.

Konkoni kuwa konki?

Mwamba Hafiz Konkoni ingizo jipya ndani ya Yanga aliyetambulishwa Julai 29 kutoka Klabu ya Bechem United ya Ghana anasubiriwa kwa shauku na mashabiki kuona kama kweli atakuwa ni konki kama jina lake.

Ni kiatu kizito anakibeba kutoka kwa Fiston Mayele aliyeongoza timu ya Yanga kutwaa Ngao ya Jamii msimu wa 2022/23 alipotupia mabao yote mawili dhidi ya Simba, Uwanja wa Mkapa.

Mayele hatakuwa ndani ya Yanga baada ya kupata dili katika Klabu ya Pyramids ya Misri. Wakati anasepa Yanga kwenye misimu miwili ya ligi alikuwa ni namba moja kwa utupiaji, msimu wa 2021/22 alitupia mabao 16 na msimu wa 2022/23 alitupia mabao 17.

Kisasi kulipwa

Oktoba 25 kwenye Ligi Kuu Bara watakutana wababe hawa ikiwa ni Mzizima Dabi ambapo wale watakaopata maumivu kwenye Ngao ya Jamii watakuwa kwenye hesabu za kulipa kisasi wakifanikiwa.

Ni Uwanja wa Mkapa ikiwa ni raundi ya Sita na wenyeji wanatarajiwa kuwa Yanga. Ile burudani ambayo itakuwa ikisubiriwa ni kujua nani atasepa na pointi tatu.

Ikumbukwe kwamba timu zote maskani yake ni Dar, Azam FC wao maskani yao ipo Azam Complex na Yanga ni AVIC Town, watoto wa mjini watakutana kuendelea pale walipoishia.

Vivuruge kwenye kapu moja

Watibuaji wa shughuli wapo kwenye kapu la kusaka ushindi. Kwa Yanga wanaye mtaalamu Kennedy Musonda aliyefunga msimu wa 2022/23 kwa kuwatungua bao moja Azam FC katika fainali ya Azam Sports Federation.

Kwa upande wa Azam FC wanaye Feisal Salum aliyewavuruga Yanga alipoomba kusepa hapo kupata changamoto mpya. Anaibukia Azam FC ikiwa atapata nafasi kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii itakuwa ni mchezo wake wa kwanza.

Nani kuanza kwa kicheko?

Yanga walianza kwa kicheko msimu wa 2022/23 walipotwaa taji la Ngao ya Jamii kwa kupeleka maumivu kwa watani zao wa jadi Simba.

Azam FC walifunga msimu kwa maumivu ya kupoteza taji la Azam Sports Federation. Huu ni mwanzo wa msimu mpya atakayeanza na kicheko huenda kasi yake ikazidi mpaka kwenye ligi.

Tambo za maofisa Habari

Ali Kamwe, Ofisa Habari wa Yanga amesema kuwa wapo tayari kufanya vizuri kwenye mechi zote za ushindani.

“Tulianza na Ngao ya Jamii msimu wa 2022/23 na msimu mpya tunahitaji kuendelea pale tulipoishia tunatambua utakuwa mfumo mpya tupo tayari,”.

Hasheem Ibwe, Ofisa Habari wa Azam FC amesema kuwa kikubwa ni kupata matokeo kwenye mechi wanazocheza.

“Tupo tayari kwa ajili ya kupata matokeo chanya na tunatambua ushindani ni mkubwa, mashabiki wajitokeze kwa wingi kuona burudani,”.

Imeandikwa na Dizo Click na imetoka gazeti la Championi Jumatano.