SINGIDA FOUNTAIN GATE WAJA NA MKWARA HUU

UONGOZI wa Singida Fountain Gate umesema kichapo cha bao 1-0 ilichokipata kutoka Coastal Union juzi ukiwa ni mchezo wa kirafiki hakuwazuii kufanya vyema dhidi ya Simba kesho Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Huo ulikuwa ni mchezo wa kirafiki kwa timu hiyo ambayo imewasili Tanga kwa ajili ya maandalizi ya mwisho ya Ngao ya Jamii inayotarajiwa kuanza leo Uwanja wa Mkwakwani.

Singida itacheza na Simba katika mchezo wa nusu fainali ya pili ya Ngao ya Jamii, mechi saa 1:00 usiku.

Ofisa Habari wa Singida Fountain Gate, Hussen Masanza amesema: “Lengo la mchezo ni kuona wapi pana mapungufu zaidi ili tuweze kupafanyia marekebisho kuelekea mchezo wetu dhidi ya Simba.

“Niwaondoe hofu Wanasingida kupoteza dhidi ya Coastal Union kusiwafanye wakate tamaa tunawaahidi mchezo mzuri na matokeo mazuri dhidi ya Simba.”

Singida Fountain Gate inafundishwa na Kocha Mkuu, Hans Pluijm ina nyota wapya ikiwa ni pamoja na Joash Onyango, Beno Kakolanya ambao hawa waliwahu kuwa ndani ya Simba.

Mbali na nyota hao waliopo Singida Fountain Gate Gadiel Michael naye alikutana na Thank You ndani ya Simba kwa sasa yupo Singida Fountain Gate.